Ijumaa , 25th Aug , 2023

Mtoto wa miaka minne katika mtaa wa uwanja kata ya Nyankumbu wilayani Geita ambaye jina lake limeifadhiwa ameunguzwa mikono yote miwili kwa moto na bibi yake anayefahamika kwa jina la Vestina Joeli kwa madai mototo huyo ameiba karanga za mboga maarufu kama kitwiri.

Mtoto huyo akiongea na EATV huku akiugulia maumivu makali amesema bibi yake alimpeleka jikoni na akaweka mikono yake kwenye mafiga ya kupikia na kuanza kumuunguza na moto huku akisema mototo huyo aache tabia ya udokozi.

Aidha Bibi huyo alipohojiwa na kituo hiki alikili kufanya kitendo hicho kwasababu ya hasira na hakufikiria kwamba kitendo alichokifanya kingeleta madhara makubwa kwa mototo huyo.

“Mimi kweli nilimuunguza lakini ilikuwa ni hasira maana niliona nikimuacha ataendelea kuiba hata kwa majirani, halafu nilimgusisha tu kwenye figa la moto sikujua kuwa angeungua hivi” amesema Vestina Joel ambaye ni bibi wa mtoto.

Editha Godfrey ambaye ni shuhuda wa tukio hilo na jirani wa familia hiyo anasema sio mara ya kwanza mtoto huyo kuunguzwa na moto na bibi yake kwani kila akila kwa jirani au kudokoa mboga adhabu yake ni kuunguzwa na moto.

“Huyo mtoto aliyeunguzwa alikuja na mia mbovu kununua sambusa nilipoona mikono yake imeungua nikamuuliza imekuwaje akasema nimeunguzwa na bibi nikamuuliza hii ni mara ya ngapi akaniambia ni mara ya tatu nikamuuliza tena kwani umefanya nini akaniambia kila nikila kwa jirani au kudokoa mboga ananiunguza nikamuuliza kwanini unadokoa akaniambia bibi anaenda sokoni asubuhi anarudi jioni kwahiyo ninakuwa na njaa” amesema Editha Godfrey

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Uwanja, Enos Chelehani amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo la mtoto kuunguzwa mikono na bibi yake kwa kosa la kudokoa karanga za mboga maarufu kama Kitwiri.

“Inasikitisha sana karanga za 300 zinamfanya bibi huyu kumfanyia mjukuu wake ukatili kama huu, sisi kama mtaa tumechukua hatua ya kumweka chini ya ulinzi mama huyo na kwa sasa yupo ofisini na muda sio mrefu tutamfikisha polisi ili sheria ichukue mkondo wake” amesema Enos Chelehani