Jumatatu , 19th Mei , 2014

Wafanyabiashara na mafundi gereji katika eneo la biafra jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, wapo hatarini kuugua magonjwa ikiwemo ugonjwa wa homa ya dengu kufuatia eneo hilo kuwa na dimbwi kubwa la maji yaliyotuama karibu na maeneo yao ya kazi.

Wakizungumza na East Africa Radio, wameiomba serikali kuchukua hatua haraka za kupuliza dawa katika dimbwi hilo la maji, kutokana na kuwepo katika eneo hilo kwa muda mrefu huku viongozi wa serikali ya mtaa wakiwa hawachukui hatua zozote.

Wananchi hao Bw. Hassan Michael ambaye ni fundi wa magari, Bw. Vincent Jackson ambae pia ni fundi wa magari pamoja na Bw. Ramadhani Ally ambae ni Mfanyabiashara katika eneo hilo la Biafra, wamesema mlipuko wa ugonjwa wa homa ya dengu unaweza kuwakumba iwapo hakutakuwa na jitihada za serikali za kuhakikisha kwamba dimbwi hilo la maji linafukiwa.