Jumatano , 9th Nov , 2016

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 200 katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuongeza mikopo itakayowasaidia wakulima wadogo kuendesha shughuli za kilimo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Ole Nasha

 

Hayo yamebainishwa mjini Dodoma leo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nashe wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mh. Rose Sekum aliyehoji kuhusu mpango wa serikali kuwafikia wakulima wadogo nchini.

“Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya Benki hiyo ambapo kwa mwaka huu tumetenga Shillingi Bilioni 200, hata hivyo tumejizatiti kuongeza mtaji kupitia Hati Fungani ya mitaji isiyo ya fedha taslimu yenye thamani ya shilingi bilioni 800”, alisema Mhe. Nashi.

Ameongeza kwamba, kufuatia ujio wa Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kumekuwa na mazungumzo baina ya benki hizo mbili kuhusu kupatiwa mkopo ambao utaiongezea mtaji Benki ya TADB ili iweze kusaidia wakulima wengi zaidi.

Wakulima wa chai

Katika utekelezaji wa mpango huo, Benki ilianza kwa kuvijengea uwezo vikundi 89 vya wakulima wadogo vyenye jumla ya wakulima 21,526 na kati ya hivyo, jumla ya vikundi 8 vilitimiza masharti ya msingi ya kuweza kukopa na vilikopeshwa jumla ya shilingi billion1.

Mpaka sasa TADB inatoa huduma za mikopo kwa wakulima katika mikoa 6 kwa kushirikiana na Sekretarieti za mikoa, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mfuko wa Pembejeo na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.