Jumatano , 6th Sep , 2023

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent L. Bashungwa amewaigiza Maneneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mikoa yote nchini kufanya upembuzi yakinifu na kubaini maeneo yote korofi ya barabara na kuyawasilisha Wizarani ili yaweze kupewa kipaumbele wakati wa kuandaa bajeti.

Mhe. Bashungwa amesema hayo leo Septemba 06, 2023 Bugeni Dodoma wakati alipota nafasi ya kujibu maswali ya wabunge kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

“Nitumie nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wa TANROADS mikoa yote kuangalia maeneo yote korofi na kufanya Upembuzi yakinifu na kuyawasilisha Wiazarani ili yapewe kipaumbele wakati wa kuandaa bajeti” amesema Bashungwa.

Awali kabla ya kujibu maswali ya wabunge hao, Waziri Bashungwa alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini huku akiahidi kudhibiti  na kupambana na Rushwa katika mikataba, manunuzi na usimamizi wa miradi.

“Ninamshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuniamini, Mimi pamoja na Niabu Waziri tunamhadi kufanya kazi kwa bidii kwa kupambana na kudhibiti Rushwa hasa kwenye maeneo ya mikataba, manunuzi na usimamizi wa miradi, ili dhamira ya Mheshimiwa Rais na Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi uende Vyema”