Jumanne , 26th Mar , 2019

Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein  Bashe ameweka wazi kwamba hatotumia tena salamu za kidini katika mikutano ya hadhara ili kutokiletea chama chake matatizo.

Hussein Bashe

Bashe ameweka wazi leo huku akieleza kwamba hatotumia tena salamu hizo ambazo zitapelekea chama cha Mapinduzi kuonekana kwamba kinabagua wasio na dini.

"Kuanzia leo nikienda kwenye mikutano ya hadhara situmii salaam kama “Assalaam Alykum” or “Bwana Yesu Asifiwe” nisije nikakiletea matatizo chama chetu CCM nakuonekana kinabagua wasiokua na dini" Bashe.

Ameongeza kwamba, “tafakuri yangu tahadhari kabla ya mauti".

Hata hivyo tafakuri hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Msajili wa Vyama, Jaji Fransic Mutungi kutishia kukifuta  Chama Cha ACT - Wazalendo kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwamo kuchoma moto bendera ya Chama cha Wananchi (CUF) huku wakitumia maneno ya kidini.

Sehemu ya taarifa ya msajili ilisema kwamba, "vile vile katika mitandao ya kijamii imeonekana video watu wakipandisha bendera ya ACT kwa kutumia tamko takatifu la dini ya kiislamu (Takbir), kitendo hiki pia ni kukiuka kifungu cha (9) (1) (c) cha Sheria ya Vyama vya Siasa inayokataza kuwa na ubaguzi wa kidini kwa wanachama wake na kifungu cha (9) (2) (a), kinachokataza katiba, sera au vitendo vya chama cha siasa kuhamasisha au kueneza dini fulani".