Jumanne , 23rd Feb , 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewasili mjini Bujumbura, Burundi katika juhudi za kujaribu kukwamua mzozo wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miezi kumi nchini humo kufuatia muhula wa tatu wa Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon akilakiwa na Makamu wa pili wa rais nchini Burundi Gaston Sindimwo mjini Bujumbura, baada ya kuwasili

Bwana Ban Ki-Moon amewasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumburajana jioni.

Kulingana na ratiba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atakuwa na mazungumzo ina wakuu wa vyama vya siasa, lakini vilevile mashirika yasiyokuwa ya serikali yanayohudumu Burundi kabla ya kukutana kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nje Alain Nyamitwe.

Aidha kulingana na ratiba hiyo Ban Ki-Moon atakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ofisini kwake asubuhi ya leo.

Viongozi hao wawili watakuwa na mazungumzo na vyombo vya habari muda mfupi kabla ya Ban Ki-Moon kuendeleza duru yake katika nchi jirani ya DRC na baadaye Sudan Kusini.

Ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi inadhamiria kukwamua mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miezi kumi kufuatia muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza.

Bwana Ban anataraji kumshawishi Rais wa Burundi kukubali mazungumzo Jumuishi na wapinzani lakini vilevile kuzungumzia kuhusu visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu vinayoshuhudiwa nchini tangu mzozo uliporipotiwa.

Katika kile kinachoonekana kama kulegeza misimamo, serikali ya Burundi imeondoa waranti 15 za kukamatwa viongozi wa kisiasa waliokuwa wanasakwa na vyombo vya kimataifa kwa jumla ya wanasiasa 34 wa upinzani.

Ni wiki hii pia serikali ya Burundi imeazimia kufungua radio 2 za binafsi na kuwaruhusu wachunguzi 25 wa kimataifa wa haki za binadamu kutoka muungano wa Afrika.