Jumatano , 1st Oct , 2025

Mke wa Balozi huyo aliripoti kutoweka kwake baada ya kupokea ujumbe wa simu kutoka kwa mumewe ambao ulimtia wasiwasi, gazeti la Le Parisien limeripoti. Simu yake ilitafutwa hadi Bois de Boulogne lakini yeye hakupatikana.

Balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa amekutwa akiwa amefariki katika hoteli ya Hyatt Regency, huko  Porte Maillot magharibi mwa Paris, kwa mujibu wa magazeti ya Le Parisien na Le Figaro jana Jumanne.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa, Balozi Nkosinathi Emmanuel "Nathi" Mthethwa, 58, alitoweka tangu Jumatatu alasiri na inaaminika aliruka kutoka orofa ya 22 ya hoteli hiyo katika eneo la 17 la mji mkuu wa Ufaransa mwendo wa saa 1 usiku Jumanne.

Polisi wa Paris na Hyatt walikataa kutoa maoni yao wakati  simu kutoka kwa Ubalozi wa Afrika Kusini hazikupokelewa.

Mke wa Balozi huyo aliripoti kutoweka kwake baada ya kupokea ujumbe wa simu kutoka kwa mumewe ambao ulimtia wasiwasi, gazeti la Le Parisien limeripoti. Simu yake ilitafutwa hadi Bois de Boulogne lakini yeye hakupatikana.

Kwa mujibu wa DW Ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Paris imesema Balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa, aliyekutwa amekufa katika hoteli ya Hyatt Regency mjini Paris jana Jumanne, alimuachia mkewe barua ya kujitoa muhanga.

Msemaji katika idara ya maswala ya kigeni ya Afrika Kusini amesema wanafahamu ripoti  hizo zinazosikitisha zinazomhusu Balozi Nathi Mthethwa na watatoa taarifa mara tu kutakapokuwa na taarifa rasmi. Mthethwa alihudhuria Maadhimisho ya Miaka 109 ya Vita vya Delville Wood huko Longueval, Idara ya de la Somme, Jumamosi.

Mthethwa aliteuliwa kuwa Balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa na Mjumbe wa Kudumu wa UNESCO mwezi Machi 2024. Mwanaharakati huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi, alijiunga na Umoja wa Vijana wa Chama cha Afrika Kusini cha African National Congress (ANC) mwaka 1990 na alichaguliwa katika Kamati yake Kuu ya Taifa mwaka 1994, ambapo alihudumu kama katibu hadi 2001.

Aliingia bungeni mwaka wa 2002 na kuteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa ANC mwaka wa 2008. Aliendelea kushikilia nyadhifa kadhaa za uwaziri kati ya 2008 na 2023, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Sanaa na Utamaduni, akiongoza michezo kwenye ofisi yake kutoka 2019 hadi 2023.