Balozi Agustine Mahiga ametangaza nia hii leo ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na kuahidi kudumisha umoja wa taifa ambao kwa kiasi fulani umeanza kuathiriwa na masuala ya ukabila, udini, ukanda na hata ubaguzi wa kirika.
Balozi Mahiga ametangaza nia hiyo leo Jijini Dar es Salaam, ambapo pia amesema licha ya taifa kuwepo katika mfumo wa vyama vingi lakini mfumo huo haupaswi kutumika kuvunja umoja wetu na kuitikisa amani ya nchi.
Aidha, Balozi Mahiga amezungumzia suala la kuachwa maadili ya viongozi na kupelekea kuwepo kwa tatizo la rushwa ambalo limefikia mahali ambapo madhara yake ni makubwa kisiasa kiuchumi pamoja na kuchangia kushusha hadhi ya taifa la Tanzania.