Jumanne , 6th Nov , 2018

Mamlaka ya Uhamiaji nchini imesema inaendelea kuchunguza uraia wa aliyekuwa Mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi nchini (TSNP), Abdul Nondo, na mchungaji Zakaria Kakobe, na hivi karibuni itaweka wazi uchunguzi.

aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP), Abdul Nondo.

Akizungumza na www.eatv.tv hivi karibuni Mratibu wa polisi, na Msemaji wa Idara ya uhamiaji Ally Mtanda amesema bado idara hiyo inaendelea na ufatiliaji wa suala la uraia wa watu hao wawili na likiwa tayari watazungumza na watuhumiwa wenyewe kuhusu taarifa zao.

Ally Mtanda amesema “ bado uchunguzi wao unaendelea na pale ambapo idara ya uhamiaji itakapojiridhisha tutaweka wazi, au tutawasiliana na watuhumiwa wenyewe, lakini lazima tupate ridhaa ya watuhumiwa wenyewe.”

Aidha Mtanda amesema zaidi ya watanzania elfu 40 wameshapatiwa hati ya kusafiria ya kieletroniki tangu zoezi hilo lizinduliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Mapema wiki hii idara hiyo ya uhamiaji ilitangaza zoezi la majaribio la kutambua vitambulisho vya uraia kwa baadhi ya wasafiri kutoka mikoa ya kigoma, Kagera, Dodoma na Mara.

Tutafanya majaribio kwa muda mfupi ili kujifunza changamoto zikoje kabla ya kutangaza agizo la nchi nzima kwa hiyo tunaenda awamu kwa awamu, kwa maeneo ambayo hawana vitambulisho wajitahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili kupata vitambulisho.” Alisema Mtanda.

Jana kupitia mahakama ya mkoa wa Iringa iliamuru kuachiliwa huru kwa kijana Abdul Nondo baada ya kutomkuta na hatia dhidi ya makosa yake mawili ikiwemo la kutoa taarifa za uongo na kosa la kujiteka.