Alhamisi , 4th Aug , 2016

Baada ya kumalizika kwa shughuli ya utatuzi wa changamoto ya madawati sasa mkoa wa Mbeya umejipanga kuelekeza nguvu zake katika utatuzi wa tatizo la upungufu wa vyoo mashuleni.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akikagua madawati

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla,mkoa una uhaba wa matundu 13,435 kwaajili ya wanafunnzi na walimu ambapo upungufu kwa shule za msingi ni 9,804 na sekondari ni 3,628.

Katika kikao cha Kazi kilichofanyika jana,Makalla na wajumbe kutoka halmashauri saba za mkoani hapa,walikubaliana kuanza utekelezaji wa changamoto hiyo mara moja na ifikapo Desemba mwaka huu vyoo view vimekamilika.

Makalla amesema ni jambo linalokosa tafsiri nzuri kwa mwanafunzi kukalia madawati mazuri darasani lakini akapata wakati mgumu anapokwenda kujisaidia chooni.

Amesema pia suala la uhaba wa vyoo limekuwa wimbo kwa kila shule kwani kila msaada unapopelekwa mashuleni wanafunzi wanaposhukuru lazima waombe kukumbukwa na upande wa vyoo.

Amesema kama jitihada shirikishi zilivyofanikisha suala la madawati ndivyo na mkakati wa kujenga vyoo unapaswa kuwekwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kuchangia kulingana na uwezo wao.