Ijumaa , 13th Jun , 2014

Chama cha Tiba asilia nchini Tanzania ATME, kimeiomba wizara ya afya na ustawi wa jamii, kuandaa utaratibu utakaoiwezesha bohari ya dawa MSD kununua dawa asili na kuzisambaza katika hospitali na Zahanati za Umma.

Waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seif Rashid. Wizara yake imeombwa kuangalia uwezekano wa kuruhusu dawa asilia zitumike katika hospitali na zahanati za umma.

Mratibu wa chama hicho Bw. Boniventura Mwalongo, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa dawa hizo ni zile zinazotengenezwa na taasisi zilizo chini ya serikali ikiwemo taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu - NIMR, Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ, pamoja na kituo cha utafiti wa tiba mbadala cha chuo cha afya na Sayansi za Tiba Muhimbili.

Kwa mujibu wa Mwalongo, hatua hiyo itaiwezesha nchi kuondokana na tatizo la ukosefu wa bajeti ya kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, lakini pia itasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa idadi kubwa ya watu.