
Wakati mkutano wa Healthy Cities ukifikia tamati kwa mwaka 2025 huko jijini Paris, Ufaransa, miji mitatu kati ya miji 74 wanachama imetambuliwa kwa mafanikio na hatua kubwa walizopiga katika kuzuia magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na majeraha.
Miji hiyo hiyo ni Córdoba Argentina, Fortaleza Brazil, na Greater Manchester Uingereza ambapo zimetunukiwa tuzo kwa mafanikio yao katika utekelezaji wa hatua madhubuti za afya ya umma, zikiwa kama mfano wa kuigwa kwa miji mingine duniani.
Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa Idara ya Mahitaji ya Kijamii ya Afya wa Shirika la Afya Duniani (WHO,) alisisitiza umuhimu wa kupambana na NCDs, hasa katika kipindi hiki cha changamoto nyingi za kimataifa. Alibainisha kuwa NCDs husababisha 80% ya vifo duniani, hivyo kuna haja ya mshikamano wa kimataifa kukabiliana na tatizo hili. Aidha, alieleza kuwa serikali za miji, hasa mameya na timu zao, zina nafasi nzuri ya kutekeleza sera madhubuti za afya kwa jamii zao.
“Kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na usalama wa barabarani ni changamoto, lakini tunapiga hatua na tunaona matokeo chanya,” alisema Dkt. Krug. Alisisitiza umuhimu wa kutumia data na ushahidi wa kisayansi ili kupima maendeleo na kuboresha sera kwa wakati.
Miongoni mwa miji ya Afrika Mashariki ikiwemo Kigali, Rwanda, imepiga hatua kubwa katika kuboresha njia za watembea kwa miguu, ikiwa ni juhudi za kuboresha afya na usalama wa mijini.
Ushirikiano wa Miji yenye Afya, unaoungwa mkono na WHO, Bloomberg Philanthropies, na Vital Strategies, unajumuisha miji 74 inayopata msaada wa kiufundi na kifedha ili kutekeleza afua za afya ya umma. Ni miji minane pekee kutoka Afrika iliyopo katika ushirikiano huu, ikiwa ni pamoja na Kigali Rwanda, na Nairobi Kenya.
Miji hii inaendelea kuchukua hatua za sera ili kuboresha mazingira ya mijini na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza, ambapo hapa nchini Tanzania tayari imeanza kuchukua hatua madhubuti kuelekea udhibiti wa magonjwa haya ikiwemo kuhamasisha ufanyaji mazoezi na ulaji mzuri. Jiji la Dar es Salaam limechukua hatua ya kufunga Daraja la Tanzanite Jumamosi moja ya kila mwezi kuruhusu wananchi wake kutumia Daraja hilo na Barabara zake kufanya mazoezi.