Jumapili , 12th Feb , 2017

Timu ya Young Africans ambayo ni Mabingwa wa Tanzania wanayoiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC leo Februari 12, 2017 inashuka dimbani nchini Comoro kucheza na Ngaye De Mbe ya nchini humo.

Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema kikosi chake kiko imara na hakuna majeruhi, hivyo kw maandalizi waliyoyafanya anaamini wataondoka na ushindi katika mchezo huo wa ugenini.

Mwambusi amesema licha ya Comoro kuwa chini kisoka, hawatawadharau wapinzani wao kwa kuwa ni timu ambayo imetwaa ubingwa nchini humo mara 4 mfululizo, hivyo anatarajia mechi itakuwa na ushindani.

Kuelekea mchezo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitakia kila la kheri Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo hatua ya awali imeanza wikiendi hii.

“Tunaitakia Wawakilishi wa nchi Young Africans ya Tanzania kila la kheri,” amesema Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi.

Wakati Young Africans inacheza, leo, Azam itasubiri mshindi kati ya Mbabane Swallons ya Swaziland na Opara United ya Botswana katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF).