
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Tatizo Yohana Mzumbwe, mkazi wa kijiji cha Masoko kata ya msoko wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mama yake wa kambo aitwaye Merry Yohana 61 mwenye ulemavu wa ngozi albiono mkazi wa Masoko kwa kumkata na panga kichwani.
Tatizo anatuhumiwa kutenda tukio hilo Oktoba 6, 2025 saa 2:00 asubuhi huko katika Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Masoko, Tarafa ya Isangati, Mkoani Mbeya, kwa kumuua Merry Yohana, ambaye pia alikuwa mkazi wa Masoko alikuwa mwenye ualbino.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza msako mkali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa majira ya usiku huko Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Masoko kuhusiana na tukio hilo.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia kuhusu mashamba ambapo mtuhumiwa alikuwa akimshinikiza Merry Yohana kugawa mashamba ya urithi yaliyoachwa baada ya baba yake kufariki.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya vijana kuacha tamaa ya kutaka kujipatia mali kwa njia zilizo kinyume na sheria. Uchunguzi unakamilishwa ili hatua nyingine zichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria.