Jumanne , 6th Nov , 2018

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye Rahel Matalaka (41), mkazi wa kijiji cha lugenge, kwa tuhuma za kumpiga hadi kumuua mtoto wake wa kiume aitwaye Maliatabu Constantine (10), mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Ikeleg, Wilayani Misungwi.

Maembe.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana, tukio hilo limetokea tarehe 03.11.2018 usiku, baada ya mama wa marehemu kuletewa malalamiko kuwa mtoto wake alikua akiangusha na kuiba maembe kwa jirani. Ndipo mtuhumiwa alipatwa na hasira na kumpiga mtoto kwa kutumia fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea mtoto kupoteza fahamu na baadae kufariki dunia.

Mtuhumiwa alipoona mtoto amepoteza maisha alimchukua na kumtundika juu ya mwembe kwa kutumia kipande cha khanga ili apoteze ushahidi ili baadae ionekane kuwa amejinyonga. Ndipo majirani walio ona tukio hilo walipotoa taarifa kituo cha Polisi.

"Polisi tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani. Mwili wa marehemu tayari umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa  ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi", amesema Kamanda Shana.