Jumamosi , 27th Mei , 2023

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimesema kuwa Baraka Mkama ambaye alitambulishwa kama wakili na kuonekana akiwazuia askari Polisi wasiwatie nguvuni  wateja wake baada ya kuachiwa huru na Mahakama sio wakili wala mwanachama wa TLS

Taarifa ya TLS imeeleza kuwa baada ya tukio hilo uongozi wa TLS uliunda kamati teule ya uchungzi wa tukio hilo na baada ya uchunguzi wamebaini mtu huyo sio wakili

Baada ya kupokea taarifa ya kamati, Baraza la Uongozi la TLS liliipitia na kuijadili, kwa hivyo, tunapenda kuwafahamisha Wanachama wote wa TLS, Wadau wa TLS na Umma wa Watanzania kwamba, TLS tumejiridhisha pasipo shaka kwamba mhusika wa tukio hilo ndugu Baraka Mkama sio wakili na sio mwanachama wa tanganyika law society.

Aidha TLS imeeleza kuwa  imepata taarifa muhimu za ziada kuhusu mtandao wa watu wasiokuwa mawakili wanaofanya kazi za uwakili (Vishoka) hivyo imeongezea muda Kamati Teule ya Uchunguzi kuendelea kufuatilia mtandao huo na kuwasilisha taarifa zake za ziada ifikapo tarehe 31 Mei 2023

Vilevile, TLS imekamilisha kuunda  kikosi kazi (Anti-Vishoka Taskforce) kitakachofanya kazi ya kudhibiti watu ambao hawastahili kufanya kazi za mawakili. Baraza la Uongozi la TLS linaomba ushirikiano toka kwa Wanachama wa TLS, Wadau wa TLS na Wananchi katika hizi juhudi za kutokomeza uhalifu huu. 

TLS inawakumbusha wananchi na wadau wake wote kila wakati kuhakiki taarifa za watu wanaoruhusiwa kufanya kazi za mawakili kwa kutumia mfumo wa utambuzi wa wakili wa Mahakama yaani e-wakili. TLS itahakikisha kuwa inalinda na kusimamia maslahi ya mawakili; itawalinda na kuwatetea wananchi dhidi ya vishoka; na kushirikiana na vyombo vya dola katika kudumisha hadhi, nidhamu na heshma ya Mawakili kama maafisa wa Mahakama wakati wote.