Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga Bw. Justus Kamugisha
Mbali na kukamatwa na noti hizo, pia kijana huyo amekutwa na vifaa vya kutengenezea pesa hizo bandia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga Bw. Justus Kamugisha amesema tukio hilo limetokea Desemba 27 mwaka huu, majira ya saa 2:00 usiku katika eneo la kituo cha basi kwenye kijiji na kata ya Kakola tarafa ya Msalala wilayani Kahama.
Amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari wa jeshi hilo wakati wakiwa katika doria ya kawaida kwenye kituo hicho cha mabasi akiwa na noti hizo bandia na kuwa kati yake noti 3 zina namba BL, 0315207, noti (32) BB 0315203, noti (21) BE 0315206 , na noti (19) zikiwa na namba BC 0315209.
Kamanda Kamugisha ameongeza kuwa licha ya kumkamata mtuhumiwa na noti hizo bandia, pia amekamatwa akiwa na bando ya karatasi , Sindano pamoja na chupa ya konyagi iliyokuwa na unga mweupe, vifaa ambavyo vinasadikiwa kutengenezea noti hizo.
Aidha kamanda Kamugisha ameongeza kuwa Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zinazo mkabili mara baada ya upelelezi wa jeshi hilo kukamilika.