Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Madema, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP Abubakar Khamis Ally amesema mtuhumiwa huyo aliwatapeli wananchi kwa kuwaahidi kuwapatia ajira kwenye Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Idara ya Usalama wa Taifa.
Amefafanua kwamba mtuhumiwa huyo hutumia mbinu ya kujifanya mtumishi wa serikali na kuwa ana uwezo wa kutoa ajira ambapo alifanya hivyo akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Hivyo ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya watuhumiwa wa utapeli hasa kipindi hiki ambacho Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP. Camillus Wambura ametangaza usaili kwa waombaji wa ajira za Jeshi la Polisi.
Katika hatua nyingine amesema Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa kosa la wizi wa pikipiki ambapo katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2024 wameiba pikipiki Ishirini na moja.
Amesema baada ya mahojiano, watuhumiwa hao walieleza kwamba pikipiki hizo husafarishwa mkoani Dar es salaam ambapo baada ya ufuatiliaji walifanikiwa kukamata pikipiki nne na mtuhumiwa anaepokea mali hizo za wizi ambae alikamatwa Mbagala jijini Dar es salaam.
Sambamba na hayo amesema katika kipindi cha miezi sita huu, Jeshi la Polisi limepata mafanikio makubwa mahakamani ambapo jumla ya kesi 180 zimepata hatia kwa washtakiwa wake kutumikia vifungo jela, faini na fidia.
Hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.