Ijumaa , 20th Jul , 2018

Taasisi ya mifupa na mishipa ya fahamu Muhimbili (MOI) imeeleza kuwa ajali za barabarani zinaendelea kuongezeka mwezi Mei hadi Juni mwaka huu licha ya mapambano ya serikali kuanzisha sheria mbalimbali za kuzingatia barabarani kwa ajili ya kupunguza na kuzuia ajali hizo.

Picha inayoonesha moja ya tukio la ajali

Ripoti kutoka kwenye taasisi ya ‘MOI’ imeonesha kuwa ajali za barabarani zinazohusisha madereva bodaboda na magari binafsi pamoja na ya abiria imeongezeka, ambapo madaktari katika kitengo hicho wanapokea idadi ya majeruhi wa ajali 17 mpaka 30 kwa siku.

Mmoja wa madaktari katika taasisi hiyo Kenedy Nchimbi amenukuliwa jana 19,julai 2018 akisema "mwaka 2015 wameorodhesha ajali 7800 na 2016, idadi ilipungua mpaka 6669, ambapo mwaka 2017/2018 idadi imeongezeka na kufikia 8283, kwa kuangalia mwezi Mei idadi ilikuwa 434 na kuongezeka mpaka 664 mwezi Juni, huku asilimia 40 mpaka asilimia 60 ni ajali zinazohusisha bodaboda”.

Aidha kulingana na takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2010-2013 magari 14,444 yalihusika kwenye ajali 9,147 na kusababisha vifo 957 na majeruhi 4,352, huku mabasi ya abiria 931 yalihusika katika ajali 723 zilizoua watu 313 na ajali za malori zikisababisha vifo 608.