Jumatatu , 26th Sep , 2022

Mahakama ya wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imemhukuhumu kifungo cha maisha jela, Alphonce Ngassa maarufu kama Dutwa mwenye umri wa miaka (51) kwa kosa la kumnajisi (kumbaka) mtoto wake wa kike (9) kwenye nyumba ya kulala wageni ya Lala Unono.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kumuweka binti yake katika nyumba hiyo na kumfanyia vitendo hivyo kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Nyamagana,  Juma Mpuya amesema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo mwishoni mwa mwaka jana ambapo jumla ya mashahidi sita akiwemo  mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho walitoa ushahidi wao katika mahakama hiyo.

Kutokana na ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo, mahakama hiyo ilijirisha pasipo kuacha shaka kwamba mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo na hivyo kumtia hatiani.

Kwa upande wake, Mwendesha mashtaka wa serikali,  Ghati Mathayo akaiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na kufanya kitendo kibaya kwa mtoto wake wa kumzaa ambaye ni mdogo na inadaiwa amemharibu sehemu zake za siri ikiwemo na kumharibu kisaikolojia kwa kumnajisi mwezi mzima.

Kutokana na ushahidi pamoja na maelezo ya mwendesha mashtaka mahakama ikamhukumu  kifungo cha maisha jela mshtakiwa huyo.