Jumatatu , 13th Mar , 2023

Hamis Pius (41), mkazi wa Itezi jijini Mbeya, amefariki dunia baada ya kuungua moto alipojifungia ndani ya chumba anacholala na mke wake aitwaye Rebelia Makoso(38) kisha kumwaga mafuta ya petroli na kuwasha moto huku wivu wa mapenzi ukihusishwa na tukio hilo.

Pichani ni miguu ya mtoto iliyoungua wakati akimuokoa mama yake kwenye moto huo

Wakati wa tukio mke wa marehemu alipiga kelele kuomba msaada kwa mtoto wake aitwaye Mkeshilishi Hamis (21), aliyekuwa chumba kingine na alifanikiwa kupiga teke mlango wa chumba na kisha kumuokoa mama yake lakini baba yake alikataa kutoka ndani na kupelekea kuungua hadi kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP) Benjamin Kuzaga, amesema kwamba tukio hilo limetokea Machi 8, 2023 majira ya saa 4:00 usiku.

"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hili ni wivu wa kimapenzi kwa wanandoa hao, lakini  mke na mtoto wa marehemu wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya, kutokana na majeraha ya moto waliyoyapata mwilini," ameeleza Kamanda Kuzaga.

Hata hivyo Kamanda Kuzaga amelalani tukio hilo na kutoa wito kwa jamii kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kuishauri jamii kutatua migogoro yao ya kifamilia na ndoa kwa kukaa meza moja ya usuluhishi badala ya kuchukua maamuzi magumu ikiwemo kutoa uhai.