Alhamisi , 15th Dec , 2016

Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Selemani Msindi maarufu kwa jina la Afande Sele amejivua rasmi uanachama wa chama hicho bila kutaja sababu wala chama ambacho atahamia.

Afande Sele

Afande Sele ambaye pia ni msanii wa hip hop nchini ametoa tamko rasmi la kujiondoa katika chama hicho leo kupitia ukurasa wake wa facebook, ambapo amesema ni kutokana na kuzingatia Katiba ya nchi ambayo inatoa uhuru kwa kila mtu kufanya mambo yake apendavyo ilimradi havunji sheria za nchi.

"....sasa kwa kuzingatia UHURU huo tuliopewa na KATIBA yetu mimi Leo natangaza rasmi kujivua uanachama wa chama cha ACT-Wazalendo na kutokua mfuwasi wa chama chochote cha Siasa bali nitabaki kuwa raia wa kawaida ndani ya nchi yetu huku nikiendelea na majukumu yangu mengine ya kimaisha mpaka hapo nitakavyoamua vingine kama nitakua na sababu ya kufanya hivyo...." imesema sehemu ya taarifa 

Afande amesema anawatakia kila la kheri waliobaki ndani ya chama hicho  huku akiwatia moyo kuendeleza harakati za ujenzi wa chama hicho ili kuleta upinzani sahihi na imara utakaosaidia kujenga taifa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Afande ameendelea kusema "....naomba ieleweke kuwa uamuzi huu'tarajiwa'sijauchukua kwa bahati mbaya hivyo naomba kila mmoja awe wa ndani au wa nje ya chama chetu aheshimu uamuzi wangu kama mimi ninavyoheshimu maamuzi ya watu wengine kwa mujibu wa KATIBA ya nchi inavyosema...Ahsanteni sana wadau tukutane MAISHANI..."