Jumatano , 15th Jun , 2016

Takriban asilimia 79 ya watanzania hawakubaliani na maamuzi ya serikali ya kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia runinga na radio.

Hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na shirika la TWAWEZA kupitia muhtasari wa matokeo ya utafiti wake: #BungeLive ambao pia unaonesha kuwa asilimia 92 ya wananchi wanaamini kuwa ni muhimu vikao hivyo virushwe moja kwa moja.

Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,815 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 29 Machi na tarehe 12 Aprili 2016.

Kati ya hao, asilimia 59 waliangalia vipindi vya Bunge kupitia runinga miezi miwili kabla ya utafiti huu kufanyika, na asilimia 57% walisikiliza vipindi vya Bunge kupitia radio.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa wananchi walikuwa wafuatiliaji wazuri wa vikao vya Bunge vilivyokuwa vikirushwa moja kwa moja. Sababu zao za msingi ni kama zifuatavyo:

• Asilimia 46 ya wananchi wanataka kuwafuatilia wabunge wao ili kuona kama wanawawakilisha ipasavyo.
• Asilimia 44 ya wananchi wanasema ni haki yao kufahamu kile kinachoendelea bungeni
• Asilimia 29 ya wananchi wanaamini zaidi matangazo ya moja kwa moja kwa sababu wanawaona na kuwasikia wabunge kwa macho na masikio yao wenyewe

Kwa mujibu wa utafiti huo, wananchi hao walipoulizwa na kama ni sahihi kutumia fedha za umma kugharamia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, asilimia 80 ya wananchi wamesisitiza kuwa matangazo hayo yana umuhimu sambamba na huduma nyingine za jamii.

• Wananchi walio wengi (88%) wanasema matangazo ya vikao vya Bunge yarushwe moja kwa moja bila kujali gharama.
• Watanzania wanaunga mkono kwa kiwango kikubwa (asimilia 75) suala la kuruhusiwa kwa vyombo binafsi vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya viako vya Bunge iwapo serikali imeshindwa kuyagharamaia.

Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, amesema: “Suala la kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge la Tanzania limezua mjadala mzito miongoni mwa watanzania.

Kupitia Sauti za Wananchi, tunaona wazi kabisa shauku kubwa ya wananchi ya kutaka kuwaona na kuwasikia wawakilishi wao bungeni kwa macho na masikio yao wenyewe.

Je, serikali iko tayari kuyapokea matakwa ya watanzania walio wengi katika jambo hili?

Ikibadilisha maamuzi yake na kurudisha matangazo haya itakua ishara nzuri ya nia yake ya kuimarisha uhusiano wa karibu zaidi kati ya wananchi na wabunge wao.”