Ijumaa , 26th Sep , 2025

Mamlaka katika nchi 14 za Afrika zimewakamata watu 260 katika msako mkali wa uhalifu wa mtandaoni ukilenga ulaghai wa kimapenzi na ngono.

Operesheni hiyo ya wiki mbili, iliyoandaliwa na INTERPOL, iliyopewa jina la Operesheni Contender 3.0, ilitekelezwa kati ya Julai 28 na Agosti 11, 2025 ambapo polisi walinasa zaidi ya vifaa 1,200 vya kielektroniki, kuzima miundombinu 81 ya uhalifu mtandaoni, na kubaini karibu waathiriwa 1,500 kote barani Africa. Kadirio la hasara iliyohusishwa na ulaghai huo ilifikia dola milioni 2.8.

Washukiwa hao wanadaiwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya uchumba kuwalaghai waathiriwa. Ulaghai wa kimapenzi ulihusisha wasifu ghushi na picha zilizoibwa, huku kesi za ulaghai wa ngono zikitaja waathirika kudaiwa kutumiwa video au picha chafu zilizowahusu.

Ghana ilirekodi idadi kubwa zaidi ya waliokamatwa, huku washukiwa 68 wakizuiliwa na dola 70,000 za fedha zilizoibwa kupatikana. Nchini Senegal, washukiwa 22 wanadaiwa kujifanya kuwa watu mashuhuri ili kuwalaghai waathirika 120. Polisi nchini Côte d’Ivoire walivunja pete ya jumbe za ngono yenye waathiriwa zaidi ya 800 waliotambuliwa.

Cyril Gout, kaimu mkurugenzi mtendaji wa huduma za polisi wa INTERPOL, alisema kuongezeka kwa uhalifu unaowezeshwa na dijiti kote barani Afrika kunaonyesha hitaji la ushirikiano wa kimataifa. "Ukuaji wa majukwaa ya mtandaoni umefungua fursa mpya kwa mitandao ya uhalifu kuwanyonya waathiriwa, na kusababisha hasara ya kifedha na madhara ya kisaikolojia," alisema.

Operesheni hiyo imeonesha jinsi ambavyo uhalifu wa mtandao umekuwa mojawapo ya matishio ya usalama yanayokua kwa kasi katika bara, na jinsi hatua iliyoratibiwa kati ya mataifa ya Afrika na washirika wa kimataifa ni muhimu ili kuwaweka watu salama mtandaoni.