Watanzania wachangamkie magari yanayotumia gesi

Jumatano , 30th Jun , 2021

Kuanzishwa kwa matumizi ya magari yanayotumia gesi asilia kumeelezwa kuwa kutainua fursa kwa uwekezaji katika nchi ya Tanzania ambapo uzalishaji wa gesi unazidi kutiliwa mkazo huku serikali ikitenga mabilioni ya fedha kusaidia uzalishaji wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya magari ya Scania Tanzania Limited, Johanna Lind

Akizungumza na kipindi cha East Africa Radio, cha Supa Breakfast Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya magari ya Scania Tanzania Limited, Johanna Lind amesema magari yanayotumia gesi asilia yatakuwa na faida katika kutunza mazingira na kupunguza hewa chafu ya (carbondioxide).

“Ujio wa magari haya ni fursa kwa uwekezaji mbalimbali kutokea hususan katika uzalishaji wa gesi itakayotumika, mabasi haya yana umuhimu katika kutunza mazingira na itasaidia kupunguza kodi kwani haina gharama kwenye uendeshaji wake, kuna tofauti kidogo kati ya magari haya yanayotumia gesi na mengine, hususan kwenye injini na ubunifu mbalimbali, tunaamini uwezo wa magari haya utakuwa mkubwa zaidi ya tunavyotegemea,” amesema Johanna.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa Kampuni hiyo Bi. Elivera Timothy amewataka Watanzania kuzichangamkia teknolojia zinazokuja kwa kasi kwani zinamsaada mkubwa katika kuinu si tu uchumi bali pia kuboresha maisha ya kizazi kilichopo na cha baadaye.

“Kwa teknelojia zinazokuja inabidi tuamke, kwasababu zinakuja na faida nyingi sana, kama tutapuuzia teknolojia hizi  itakuwa janga kubwa kwa kizazi chetu ambacho kipo sasa, kwa mtu yeyote mwenye gari nina muasa achukue hatua sasa kwamba kuna gesi ambayo anaweza akaipata kwa bei ndogo, atakuwa ana ‘operate’ (endesha) gari yake kwa bei ndogo huku anaokoa mazingira na kizazi chake,” amesema Elivera.