Jumapili , 20th Nov , 2022

Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha na Mipango ya Tanzania Dkt. Charles Mwamaja amesema kwamba serikali inapanga kuelimisha asilimia 80 ya watu ili kufahamu maswala ya fedha ifikapo 2025 kupitia utekelezaji wa mpango wa elimu ya kifedha.

Akiongea na wanahabari mjini Dodoma kuelekea Wiki ya Pili ya Huduma za Kifedha ya Kitaifa iliyofanyika jijini Mwanza, Dkt. Mwamaja amesema kuwa asilimia zaidi ya 40 ya wananchi hawana elimu ya masuala ya fedha licha ya jukumu kubwa la shughuli za kifedha katika maendeleo ya taifa.

Dkt. Mwamaja ameongeza kuwa ujuzi wa masuala ya fedha umesaidia mtu kuwa na usimamizi wa fedha binafsi kama vile bajeti za kaya, kadi za mikopo, bima, bajeti ya serikali, kukopa, kukopesha, kuwekeza, kodi na huduma za mikopo. Pia amesema ujuzi huo ni muhimu kwa maendeleo shirikishi na yenye maana ya kijamii na kiuchumi ya nchi husika kwa misingi endelevu.