Jumanne , 20th Sep , 2022

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inawawezesha wavuvi wadogowadogo kwa kuwapatia elimu ya uvuvi endelevu na kuzitaka halmashauri kuondoa tozo kubwa kwa wavuvi wadogowadogo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  amesema hayo katika uzinduzi wa mpango kabambe wa sekta ya uvuvi 2021/2022 – 2036/2037 Jijini Dar es Salaam, na kuwaagiza viongozi wa wizara sekta ya uvuvi, wakuu wa mikoa na wilaya kuwawezesha wavuvi wadogowadogo kwa kuwapa elimu ya uvuvi endelevu pamoja na kuona namna ya kuondoa shuru mbalimbali kwenye halmashauri zinazowarudisha nyuma wavuvi kiuchumi.

“Nitoe maagizo kuhusu swala la shuru mbalimbali za halmashauri, zisiwe kubwa na nyingi kwasababu tumegundua hizi tozo ndizo zinapelekea wavuvi wadogo katika nchi yetu kuikimbia sekta hii na kukwamisha maendeleo ya uchumi. Lengo ni kuhakikisha ndani ya miaka 10 tuweze kuchangia 10% ya pato la taifa badala ya 1.8% ambayo sekta ya uvuvi inavhangia hivi sasa"- Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Aidha, Waziri mwenye dhamana ya uvuvi nchini Mhe. Mashimba Ndaki amesema katika mpango huu wa miaka kumi katika sekta ya uvuvi wamejizatiti kuongeza wawekezaji huku M/kiti wa umoja wa wavuvi akiweka wazi changamoto wanazokutana nazo. 

Sekta hii ya uvuvi ambayo inatajwa kuchangia asilimia 1.8 ya pato la taifa imetoa ajira takribani laki mbili kwa wavuvi wadogo na wadau wengine wapatao Milioni 4.5 nchini, huku ikigubikwa na changamoto lukuki licha ya kuchangia katika upatikanaji wa kipato na usalama wa chakula.