Wanawake watakiwa kuchangamkia fursa za kifedha

Ijumaa , 9th Oct , 2020

Wanawake nchini wametakiwa kuondokana na fikra kandamizi za mfumo dume ambao huwafanya kuhisi kutokuweza kufanya chochote kwa maendeleo hivyo wametakiwa watumie fursa zilizopo katika sekta ya fedha ili kukuza uchumi wao.

Gloria Njiu Mkuu wa kitengo cha huduma cha kidigitali, NCBA.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Mussa Juma katika jukwaa la wanawake la kifedha Tanzania kwa mwaka wa pili linaloratibwa na benki ya NCBA ikishirikiana na asasi nyingine za kifedha kwa lengo la kuwainua wanawake katika sekta za kifedha na kiuongozi.

Akizungumza kwa niaba ya taasisi za kifedha nchini, Bi. Gloria Njiu, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kidigitali cha benki ya NCBA, amesema benki hiyo inahamasika zaidi kuwashika wanawake mkono katika sekta za kifedha na pia imeboresha zaidi huduma zao kwa kuwaletea huduma hizo kiganjani kwa ushirikiano na M-Pawa

Benki ya NCBA inashiriki kwenye Jukwaa la Wanawake la Kifedha linalofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam ambapo usiku wa leo kunashuhudiwa utoaji wa tuzo kwa wanawake waliofanya vizuri katika sekta ya biashara na uchumi hapa nchini.