Jumapili , 26th Feb , 2023

Balozi wa Heshima wa Jamhuri ya Slovakia nchini Tanzania Mhe. Moustafa Khataw ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za kiuchumi kwa kushirikiana na wenzao wa nchi hiyo ambao wameonesha nia ya dhati ya kutaka kuwekeza Pamoja kufanya biashara na Tanzania.

Khataw ameyasema hayo katika wakati wa kongamano la uwekezaji na biashara la Umoja wa Nchi za Ulaya lililofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Amesema Slovakia, iliyojipatia uhuru wake Januari 1, 1993 baada ya kuvunjika kwa amani umoja wake na Czechoslovakia, ni nchi iliyoendelea na yenye uchumi wa hali ya juu wa kipato, ikishika nafasi ya 45 katika Kielelezo cha Maendeleo ya Kibinadamu.

“Kuvurugika kwa uchumi katika maeneo yao kutokana na mgogoro wa Urusi na Ukraine wenzetu hawa wa Slovakia wameamua kugeukia Afrika kuendeleza shughuli zao za biashara na uzalishaji na wamevutiwa mno na Tanzania kwa kuwa nchi ya amani na vivutio vyema vya uwekezaji”, amesema Khataw.

Khatawa amesema jumla ya makampuni 18 toka Slovakia yamehudhuria kongamano hilo la biashara la EU lililofunguliwa siku ya Alhamisi na Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango na kufungwa siku ya Ijumaa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Pamoja na mambo mengine, amesema makampuni kadhaa yamedhamiria kuwekeza nchini Tanzania katika Nyanja mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa nyumba bora za bei nafuu na uzalishaji wa mbolea halisi.

Amesema Slovakia pia ni wazalishaji wakuu wa magari kwa kila mtu duniani, ambapo ilitengeneza jumla ya magari milioni 1.1 mwaka wa 2019, ikiwa ni asilimia 43 ya jumla ya pato lake la kiviwanda.