Alhamisi , 12th Sep , 2024

Serikali imepata jumla ya shilingi Trilion 1.877 kutoka  kwenye kampuni 44  zilizolinganishwa katika sekta ya madini, mafuta na gesi ikiwa na tofauti ya kati ya malipo na mapato ya shilingi milioni 402.41 kwa mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde, katika uzinduzi wa ripoti ya 14 ya Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mavunde amesema kati ya kampuni hizo, kampuni 26 ni za madini, kampuni saba ni za gesi asilia na mafuta na kampuni 11 ni kampuni zinazotoa huduma katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia. 

Waziri Mavunde ameelekeza, tofauti hiyo shilingi milioni 402 kufanyiwa uchambuzi wa kina ili kujua visababishi vilivyosababisha kutofautiana ili Kamati iweze kuzipa makampuni na serikali.
Amesema, pamoja na masuala mengine yaliyomo ripoti hiyo ya  TEITI pia imeweka wazi taarifa mbalimbali ili kutekeleza matakwa ya viwango vya kimataifa vya EITI pamoja na sheria inayosimamia shughuli za TEITI nchini. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameipongeza serikali kwa kutoa taarifa ya wazi ya ulinganisho wa mapato yatokanayo na sekta ya uziduaji na kutumia fursa hiyo kuwataka watanzania waipitie na kuona namna ambavyo sekta hii ya uziduaji inavyochangia kukuza uchumi wa nchi na kuwataka pia wananchi kutumia taarifa hii kushauri na kutoa maoni yao.