Ijumaa , 3rd Jun , 2022

Chama cha wavuvi nchini TAFU kimeiomba serikali kuingilia kati mabadiliko ya bei za uuzaji wa samaki viwandani zilizoporomoka kutoka elfu kumi na moja hadi kufikia elfu saba kwa kilo moja.

Mwenyekiti wa Chama cha wavuvi TAFU Bakari Kadabi

Mwenyekiti wa Chama cha wavuvi TAFU Bakari Kadabi ametoa ombi hilo jijini Mwanza na kusema kuwa kuporomoka kwa bei hiyo kunaweza kusababisha ongezeko la uvuvi haramu kutokana na wavuvi wengi kupata hasara kubwa.

‘Bei za Samaki zimeshuka sana kupita kiasi, kiasi kwamba wavuvi wetu wanapata hasara kubwa sana ukilinganisha bei za mafuta nazo zipo juu uendeshaji upo juu na bei zimeshuka viwandani kwahiyo ni hasara kwa wavuvi wetu"

"Matatizo ya wafanyabishara wa Samaki ndani ya viwanda yamekuwa yakishughulikiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi tunaona ipo haja kwa Wizara ya viwanda na biashara kuhusika kwenye hilo" - ameeleza Kadabi

Katika hatua nyingine Kadabi amesema sasa ni muda muafaka kwa Wizara kuunda bodi ya pamoja itakayosaidia kufuatilia bei katika masoko makubwa ya kimataifa ili kupata bei elekezi.
Changamoto ya kupanda kwa bei katika viwanda vya samaki imetokea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia mwezi wa tano.