Mitambo ya TPDC
Mradi huo ujulikanao kama Eyasi-Wembele unatatekelezwa katika Mikoa ambayo Mto huo unapitia ikiwemo Bonde la Ziwa Eyasi na Bonde la Mto Manonga unaopatikana katika Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Manyara.
Akitambulisha Mradi huo kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga, Mtaalam Mshauri wa Mradi huo Dkt Allan Mzengi kutoka TPDC, amesema kuwa mradi huo unaanza na hatua ya awali ya kuangalia athari za kimazingira katika Wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga hatua itakayoshirikisha wadau kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kata.
Dkt Mzengi ameongeza kuwa licha ya kuangazia suala la kimazingira, hatua ya pili ya mradi huo itakuwa ni ujenzi wa Mkuza katika eneo ambalo mradi huo utatekelezwa na baadaye kuweka vilipuzi vitakavyosaidia kubaini maeneo ya ujenzi wa visima vya majaribio ya utafutaji mafuta katika eneo la mradi.
Kwa upande wake Mjiolojia kutoka TPDC Gaston Canuty, amesema kuwa tayari TPDC imeishachimba visima vifupi katika eneo la mradi ili kubaini miamba yenye uwezekano wa kuhifadhi mafuta na sasa mradi huo unakusudia kwenda mbali zaidi, kuangalia mafuta yako wapi chini ya ardhi baada ya kubaini miamba hiyo katika eneo la Kishapu.
Utafiti wa Mafuta katika eneo la mradi ulianza kwa kutumia Ndege ya utafiti ambayo iliwawezesha kuona maeneo yenye miamba yenye tabaka gumu na ile ya tabaka laini na kwa kanuni za kijiolojioa maeneo yale ambayo yana mkandamizo mkubwa wa miamba ndiyo yatakayofanyiwa jaribio la utafutaji mafuta.