Ijumaa , 17th Jun , 2022

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) kuisimamia ipasavyo Taasisi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo

Amesema usimamizi huo utasaidia kuongeza ubunifu na ufanisi katika kuihudumia Serikali kwenye ununuzi wa magari, mafuta na Kugomboa na kuondosha mizigo ya Serikali kutoka bandarini, viwanja vya ndege na mipakani ili kuongeza tija.

Bi. Omolo ametoa maelekezo hayo wakati akizundua Bodi mpya ya Ushauri ya Wakala huo Jijini Dar es Salaam ambapo amesema GPSA imepewa majukumu hayo na Serikali ili iweze kuihudumia lakini kuna changamoto kadhaa ambazo Wakala huo unatakiwa kuzifanyia kazi.

Alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa Wakala huo ni kuisaidia Serikali kupunguza gharama za uendeshaji kwa kujiendesha kwa faida lakini pia kupata huduma muhimu kama upatikanaji wa magari yanayoagizwa na wakala kwa niaba ya Serikali kwa wakati, kusogeza huduma za upatikanaji wa mafuta maeneo mbalimbali ili iweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Bi. Omolo ameipongeza Taasisi hiyo inayosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kubuni mfumo wa utoaji mafuta ya magari ya Serikali ambao umeonesha ufanisi ambapo madereva wa Serikali wamekuwa wakipatiwa token ambazo huzitumia kujaza mafuta kwenye kituo chochote cha Mafuta cha GPSA hatua iliyoondoa usumbufu kwa madereva wa kutembea na makaratasi ya vibali.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini Dkt. Geraldine Rasheli alitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za GPSA na kubainisha kuwa, pamoja na mambo mengine, Wakala huo unaangalia uwezekano wa kujenga vituo vya gesi kwa ajili ya matumizi ya magari ya Serikali ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji na kupanda kwa bei za mafuta duniani.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Bi. Dorothy Mwanyika, ameihakikishia Serikali kwamba Bodi yake itasimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kuleta ubunifu na mikakati mipya itakayosaidia kuboresha utoaji huduma kwa wateja wake.

Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini ni kama duka la Serikali na malengo ya kuanzishwa kwake yalikuwa ni Kutoa huduma toshelevu ya vifaa/bidhaa kwa ubora na bei shindani; Kuandaa na kutoa orodha ya wazabuni wa vifaa na huduma mtambuka; Kugomboa na kuondosha mizigo ya Serikali kutoka bandarini, viwanja vya ndege na mipakani; na Kutoa huduma ya kuhifadhi mali na vifaa kwa kutumia maghala na maeneo ya wazi.