Alhamisi , 22nd Sep , 2022

Wakati raia wakiendelea kulalama juu ya kupanda kwa bei ya nafaka, wakulima na wafanyabiashara huenda wakawa miongoni mwa watu walionufaika zaidi na zao la mahindi baada ya bei ya jumla ya zao hilo kupanda zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mahindi yakiwa yanafungashwa

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya Agosti 2022 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2022 ilikuwa Sh87,383 ikipanda kutoka Sh43,371 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Hiyo ikiwa ni sawa na kusema kwamba, wakulima na wafanyabiashara wameweka mfukoni Sh44,012 zaidi kwa kila gunia moja au sawa na kusema bei hiyo ya mahindi imeongezeka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na bei ya mwaka jana, huku ripoti hiyo ikieleza kuwa kupanda kwa bei ya mahindi kumechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo, hasa nje ya nchi na kutokuwepo kwa mvua za kutosha katika msimu huu, jambo lililosababisha wakulima kupata mazao kidogo.

“Kuongezeka kwa bei kumechangiwa na mahitaji makubwa ya nchi jirani na kushuka kwa mavuno kutokana na mvua chache,” imeeleza BoT katika ripoti hiyo ambayo inapatikana katika tovuti yake.