Dance 100% ni shindano la nguvu kinoma ambalo huandaliwa na kituo cha television cha EATV na hufanyika kila mwaka kwa muda maalum uliopangwa.
Shindano hili lipo kimtaani zaidi, maana hutembelea mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kuweka vituo vyake kwaajili ya kufanya usajili wa makundi ya wachezaji (dancers) ambao wanapenda kucheza, kisha baada ya hapo hufanya mchujo katika vituo hivyo na kuchukua makundi matano ya washindi toka katika kila kituo na kuwapambanisha pamoja.
Lengo kuu la shindano hili ni kuwakutanisha vijana mbalimbali wenye uwezo wa kucheza ,na kisha kuwafanya wajulikane na watu tofauti kupitia kipindi hiki.
Washindi wanaopatikana katika shindano hili huzawadiwa fedha taslimu na zawadi nyinginezo kama zipo, kwa kuwapa zawadi washindi hawa huwafanya waweze kununua vifaa mbalimbali wanavyoviitaji katika sanaa yao na pia kuweza kufanya mambo yao mengine tofauti.
Washiriki katika shindano hili hucheza nyimbo mbalimbali zikiwemo reggae, R&B, Hip Hop na nyinginezo, na pia ili mtu aweze kushiriki anapaswa awe na kikundi cha wenzake kuanzia watu 5 hadi 8, mwenye afya njema, umri wa kuanzia miaka 18 (kama ana chini ya miaka hiyo anapaswa aje ana kibali toka kwa wazazi)