Wednesday , 15th Apr , 2015

JESHI la polisi mkoani Arusha, limefanikiwa kumuua jambazi sugu, George Steven Mtoso kwa jina maarufu “G”, (21) mkazi wa Murieti, Manispaa ya Arusha, wakati alipojaribu kutoroka katika uoneshaji wa bastola anayomiliki na kuwashikilia watu watatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Liberatus Sabas.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda Polisi, Liberatus Sabasi, amesema jambazi hilo lilikamatwa eneo la Daraja mbili, usiku wa April 13 mwaka huu na alipohojiwa kuhusiana na matukio aliyofanya, Kijenge nyumbani kwa Esta Mwamfule, ambapo alivunja nyumba na kuiba TV, Flat Screen na simu ya kiganjani Aprili 9 mwaka huu alikiri.

Mtuhumiwa huyo pia alikiri kuhusika katika wizi wa kuvamia nyumba ya mkazi mmoja wa Njiro na kupora bunduki yenye namba za usajili 9973 na dola za marekani 1,800.

Amesema Polisi baada ya kupata taarifa za matukio hayo walianza kumfuatilia na alipokamatwa, pia alikiri kuiba bunduki hiyo na kuwapeleka Polisi alikoificha eneo la Lemara ambako alificha nyumbani kwa Neema Adam (31).

Kamanda Sabasi amewataja watuhumiwa wengine waliokutwa eneo ilipokuwa silaha ni Erick Ombeni Palangyo (22) na Elibariki John (18), wote wakazi wa Sinoni.

Amesema lakini chanzo cha Polisi kumpiga risasi ni pale alipojaribu kuwarubuni akawaoneshe bastola anayomiliki na wakiwa njiani alijaribu kukimbia na Polisi wakampiga risasi za miguuni na baridi ikamwingia na kufariki, akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Mkoa Mount Meru,” alisema Sabasi.

Sabasi amesema jambazi hilo pia lilifungwa magereza na alimaliza kifungo chake Machi 30 mwaka huu na aliporejea uraiani alianza kuratibu makundi ya uhalifu.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti, kwenye hospitali ya mkoa, Mount Meru.