Monday , 30th Mar , 2015

Rais wa Zimbawe na Mwenyekiti wa umoja wa Afrika Robert Gabriel Mugabe amewataka viongozi wa nchi za Africa kukataa kuwa vibaraka wa mataifa tajiri duniani na badala yake wajitoe katika kuwatumikia waafrika ili kufikia mafanikio ya kimaendeleo.

Rais wa Zimbawe na Mwenyekiti wa umoja wa Afrika Robert Gabriel Mugabe.

Rais Mugabe ametoa mwito huo wakati akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa viongozi Vijana kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika na China unaofanyika katika ukumbi wa mikotano wa Ngurdoto nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Mara  baada ya kuwasili katika kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro na kupokelewa na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mohamed Gharib Billal pamoja na maofisa wengine wa ngazi za Juu kutoka mataifa ya Tanzania na Zimbabwe Kiongozi huyo wa Umoja wa Afrika AU pia amepata wasaa wa kushuhudia vikundi mbalimbali vya Ngoma Kiwanjani hapo

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano huo Rais Mugabe ametumia muda mwingi kuwaasa na kutoa mwito kwa viongozi hao vijana akisistiza kuwa Bara la Afrika linategemea mchango wa Fikra zinazojali uwajibikaji na nidhamu ya hali ya juu katika utumishi

Awali akizungumza katika Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete ameonesha imani aliyonayo kupitia mkutano wa viongozi vijana kutoka Afrika na Uchina kwamba utatoa fursa ya kutoka na maazimio yatakayokuwa na tija kwa mustakabali wa watu wote.

Kwa upande wao Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa CCM Taifa  Sadifa Hamis  pamoja naye Mwenyekiti wa mkutano huo Steven Masele wameeleza namna vijana wa Afrika watakavyonufaika na fursa watakazozitengeneza hasa katika sekta ya viwanda na biashara lakini pia uimarishwaji wa uhusiano ili kufikia maendeleo ya kiuchumi katika barani Afrika.

Mkutano huo umeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na chama cha kikomunisti cha nchini China ambapo unawakutanisha viongozi vijana wa barani Afrika na China lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano na kubainisha huku shauku kubwa ikiwa ni kwa namna gani uchina taifa lililoendelea zaidi inaweza kuisaidia Afrika kupiga hatua kubwa zaidi katika biashara na viwanda.