Thursday , 23rd Apr , 2026

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma, amesema kuwa wabunge wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kuwaelimisha wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta duniani, badala ya kuihamishia serikali mzigo wa lawama.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma, amesema kuwa wabunge wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kuwaelimisha wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta duniani, badala ya kuihamishia serikali mzigo wa lawama. 

Ametoa kauli hiyo leo Aprili 23, 2026 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati Bungeni jijini Dodoma.

Msukuma amesema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni janga la kimataifa linalotokana na misukosuko ya soko la dunia, hivyo ni muhimu kwa wabunge kueleza ukweli huo kwa wananchi wanaowawakilisha. 

Amesisitiza kuwa Bunge ndilo lenye mamlaka ya kufanya marekebisho ya bajeti, hivyo wabunge wanaotaka kupunguza kodi au gharama za mafuta wanapaswa kuonesha maeneo ya kupunguza badala ya kutoa shinikizo kwa serikali.

Akimpongeza Waziri wa Nishati kwa kuonesha ukomavu katika kusimamia sekta hiyo, Msukuma amesema kuwa changamoto za kimataifa zinahitaji uthabiti na uongozi wa pamoja, si lawama. 

Amebainisha kuwa hatua yoyote ya kupunguza bei ya mafuta bila mpango mbadala inaweza kuathiri miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami unaoendelea kwa mara ya kwanza katika jimbo lake.

Katika hatua nyingine, Msukuma amesema kuwa, tayari ana mkutano na wananchi wake leo, ambapo atawapa ufafanuzi kuhusu sababu za kupanda kwa bei ya mafuta na umuhimu wa kukubaliana na hali hiyo kwa muda. 

Amesisitiza kuwa wabunge wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu sahihi kwa wananchi ili kulinda utulivu na maendeleo ya taifa.