Tuesday , 17th Feb , 2026

Mwezi kama huu, miaka 30 iliyopita, ulimwengu wa muziki ulishuhudia tukio kubwa la kihistoria — kuachiwa kwa album ya kipekee ya rap, All Eyez on Me kutoka kwa rapa nguli Tupac Shakur.

Album hii ilitoka rasmi Februari mwaka 1996 chini ya lebo ya Death Row Records, na mara moja ikawa gumzo duniani kote. Ikiwa ni album ya kwanza ya rap kuwa na diski mbili (double album) katika historia ya hip hop wakati huo, All Eyez on Me iliweka viwango vipya vya mafanikio kibiashara na kisanii.

Ndani yake kulikuwa na mchanganyiko wa nyimbo kali zilizoonesha umahiri wa Tupac katika uandishi, mtiririko (flow), na uwezo wake wa kugusa hisia za wasikilizaji. Nyimbo kama “California Love,” “Ambitionz Az a Ridah,” na “How Do U Want It” ziliifanya album hii kuwa moja ya kazi zenye ushawishi mkubwa katika historia ya hip hop.

 

Miaka 30 baadaye, All Eyez on Me bado inatajwa kama moja ya album bora kabisa kuwahi kutolewa katika muziki wa rap. Iliuza mamilioni ya nakala duniani na kuendelea kuwa rejea muhimu katika mjadala wa album bora za muda wote.Kwa wengi, kazi hii ilithibitisha kuwa Tupac hakuwa tu rapa, bali alikuwa msemaji wa kizazi sauti ya mitaani iliyoweza kufika dunia nzima.

Kuachiwa kwa All Eyez on Me mwaka 1996 hakukuwa tukio la kawaida, bali ilikuwa ni alama ya mabadiliko katika historia ya muziki. Leo, tunapokumbuka miaka 30 ya album hii, tunasherehekea si tu muziki wake, bali pia mchango wake mkubwa katika utamaduni wa hip hop duniani.