Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Fahima Yasin Twaibu (19), mfanyakazi wa ndani na mkazi wa Mtaa wa Balyehela, Kata na Wilaya ya Ilemela, kwa tuhuma za kutupa kichanga cha kike kinachokadiriwa kuwa na umri wa takribani masaa mawili tangu kuzaliwa.
Tukio hilo linadaiwa kutokea tarehe 25 Desemba 2025 majira ya saa 11:00 alfajiri katika Mtaa wa Balyehela, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kutupa kichanga hicho muda mfupi baada ya kujifungua juu ya paa la nyumba inayomilikiwa na Emmanuel Magina Murul, fundi wa kuchomelea vyuma na mkazi wa eneo hilo.
Askari Polisi kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii pamoja na wananchi walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuokoa maisha ya kichanga hicho, ambacho kilikimbizwa Hospitali ya Mkoa Sekou-Ture kwa ajili ya matibabu zaidi.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa, ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Aidha, Polisi imetoa wito kwa jamii kushirikiana kwa karibu katika kulinda haki na maisha ya watoto, ikisisitiza kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni kosa la jinai.

