Mkuu wa Idara ya Maboresho ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) wakili Harold Sungusia.
Ufafanuzi huo ni pamoja na vipengele tata katika sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, ikiwemo hoja ya mamlaka ya kusitisha bunge hilo, kama ambavyo imekuwa ikizungumzwa na wadau wengi.
Mkuu wa idara ya maboresho wa LHRC wakili Harold Sungusia amesema hayo leo Jijini Dar es salaam ambapo amepinga dhana nzima ya kwamba Rais hana mamlaka ya kulivunja bunge hilo, kama mwanasheria mkuu Jaji Frederick Werema alivyoeleza mwishoni mwa wiki katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Aidha, wakili Sungusia amemtaka Werema kulisaidia taifa kwa kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu katika sheria ya mabadiliko ya Katiba kikiwemo kifungu cha 25 kuhusu mamlaka kamili ya bunge maalumu la Katiba kwa maelezo kuwa watu wasio na nia njema wanaweza kukitumia kifungu hicho kwa maslahi binafsi na yanayoweza kuligharimu taifa.
Hapo jana, Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, Mhe. James Mbatia alielezea kushangazwa na kile alichokiita kuwa ni upindishaji wa sheria juu ya uhalali wa kusitishwa au kutositishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Akizungumza wakati akitoa maazimio ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana jijini Dar es Salaam; Mhe. Mbatia ameonesha kushangazwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kuwa hakuna mwenye uwezo wa kusitisha bunge hilo.
Aidha, Mbatia amehoji ni wapi bunge hilo lilipata uhalali wa kisheria wa kusitisha vikao vyake na kupisha vikao vya bunge la bajeti, huku ishara zikionesha kuwa bado bunge hilo litahitaji muda zaidi ya ule uliomo kwenye sheria wa kuendelea na mchakato wa katiba mpya.