Wednesday , 3rd Dec , 2025

Papa Leo ameutaka utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kutojaribu kumwondoa madarakani Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kwa kutumia nguvu za kijeshi.

Leo, Papa wa kwanza raia wa Marekani, alisema itakuwa bora kujaribu mazungumzo au kuweka shinikizo la kiuchumi kwa Venezuela ikiwa Washington inataka kuona mabadiliko huko.

Alipoulizwa wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu vitisho vya Trump vya kumuondoa Maduro kwa nguvu, Leo alisema: "Ni bora kutafuta njia za mazungumzo, au labda shinikizo, ikiwa ni pamoja na shinikizo la kiuchumi."

Papa, akizungumza wakati akirudi nyumbani kutoka ziara ya Uturuki na Lebanon, safari yake ya kwanza nje ya nchi, aliongeza kuwa Washington inapaswa kutafuta njia nyingine za kufikia mabadiliko "ikiwa ndio wanataka mabadiliko."

Shirika la habari la Reuters liliripoti mwezi uliopita kwamba Marekani inafikiria kufanya jaribio la kumpindua kiongozi huyo wa Venezuela, na jeshi la Marekani liko tayari kwa awamu mpya ya operesheni baada ya kuongeza wanajeshi katika Caribiani na karibu miezi mitatu ya mashambulizi dhidi ya boti zinazoshukiwa za biashara ya madawa ya kulevya katika pwani ya Venezuela.

Leo, akijibu swali la mwandishi wa habari, pia alisema ishara zinazotoka kwa utawala wa Trump kuhusu sera yake kuelekea Venezuela haziko wazi.

Papa, aliyechaguliwa mwezi Mei kutoka Chicago, anaifahamu Amerika ya Kusini kwa sababu alikaa miaka mingi kama kasisi nchini Peru.