Saturday , 4th Oct , 2025

Ulishawahi kujiuliza kwa nini mabilionea na matajiri wengi duniani hawaweki majina yao kwenye mali wanazomiliki? Huu siyo uoga, bali ni mchezo wa akili na mkakati wa hali ya juu. 

 

Kabla hatujaenda mbali, unakumbuka kisa cha kushtua cha mwanasoka Achraf Hakimi? Hebu fikiria kama mali zote zingekuwa zimeandikwa kwa jina lake. Kisa kile ni mfano mdogo tu wa picha kubwa.

Hizi ni baadhi ya sababu kuu zinazowafanya matajiri wasimame nyuma ya pazia:

1. Kanuni ya Dhahabu: Hawamiliki, Wanadhibiti (Control)

Hii ndiyo siri kubwa zaidi. Matajiri wakubwa hawalengi "kumiliki" mali, bali "kudhibiti" mifumo. Unaisikia familia ya Rockefeller ikiwa na nguvu kubwa kwenye uchumi wa dunia, lakini huwezi kutaja mali mahususi wanazomiliki moja kwa moja. Mwenye control ndiye mwenye nguvu, si lazima awe mmiliki kwenye makaratasi.

2. Kujenga Ngome dhidi ya Mashambulizi

Pesa na mafanikio huvutia maadui. Ikiwa biashara na mali zako zote ziko wazi kwa jina lako, inakuwa rahisi kwa washindani, wadai, au hata watu wenye nia mbaya kukulenga na kukufilisi. Kwa kuficha umiliki, wanajenga ngome ya kisheria ambayo ni vigumu kuipenya.

3. Mchezo wa Kisaikolojia Kibiashara

Hapa ndipo akili nyingi hutumika. Tajiri anaweza kumiliki kampuni ya simu 'X' na kampuni pinzani 'Y'. Wewe unaweza kuichukia kampuni 'Y' kwa sababu ya stori ulizowahi kusikia kuhusu mmiliki wake, na kwa mapenzi yote ukanunua bidhaa za kampuni 'X', bila kujua kuwa pesa yako inaishia kwenye mfuko wa mtu yuleyule. Huu ni ushindi wa kimya kimya.

4. Faragha na Usalama: Kutoweka Lengo Mgongoni

Umaarufu wa utajiri ni sumaku ya hatari. Unavutia wezi, watekaji nyara, matapeli, na vitisho. Kwa kutojionyesha kama mmiliki wa mali nyingi, tajiri analinda usalama wake na wa familia yake. Ni rahisi kuishi kwa amani ukiwa hauonekani kama "shabaha nono".

5. Kuepuka Jicho la Husuda na Chuki

Katika jamii, kuna watu ambao huendeleza chuki dhidi ya waliofanikiwa. Ili kuepuka chuki zisizo na msingi na njama za kijamii, matajiri wengi huamua kutoweka mali zao hadharani, wakigawa umiliki katika majina na taasisi mbalimbali.

Mambo Mengine ya Kuzingatia Pia, kuna masuala ya kodi, mikakati ya kisiasa, na kurithisha utajiri kwa vizazi vijavyo bila mivutano.

 

ONYO MUHIMU: Ingawa hii ni mbinu yenye nguvu, inakuwa hatari sana ikiwa utajiri huu utafichwa hata kwa familia yako ya karibu. Siri kama hii inaweza kusababisha maafa na migogoro mikubwa pale ambapo muhusika anapoondoka duniani.