
Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Kisarawe Mkoani Pwani Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameeleza kuwa kujengwa kwa Kongani la Viwanda na uzinduzi wa Bandari Kavu Kwala Mkoani Pwani kutafanikisha Ujenzi wa viwanda 200 katika eneo hilo kwa uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 3, suala ambalo litawezesha mauzo ya mwaka ya Dola za Marekani Bilioni 6, 2 zikiwa mauzo ya nje na Dola Bilioni 4 zikiwa mauzo ya bidhaa mbalimbali ndani ya Tanzania.
Wakati wa uwekaji wa Jiwe la msingi kwenye Kongani la Viwanda Kwala kulikofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Jafo amebainisha kuwa Kongani hiyo pia itawezesha kutengeneza ajira 300,000 ikiwemo ajira za Moja kwa moja 50,000, suala ambalo litawezesha kuzalisha ajira kwa Vijana wa Pwani na Tanzania kwa Ujumla.
"Unaibadilisha nchi yetu kutengeza ajira kwa vijana na takwimu za vijana wanaomaliza elimu ya Vyuo vikuu imeongezeka. Mwaka 2021 graduate walikuwa 51, 800 leo hii wamefika 57,000 sasa hivi dunia nzima, sekta binafsi ndiyo sehemu pekee ya kuajiri watu wengi na Dkt. Samia unaifanya hiyo kazi, sisi wana Pwani na Wizara ya Viwanda na biashara tutasimamia maono yako kwa wivu mkubwa kuhakikisha nchi yetu inakuwa kinara kiuzalishaji wa bidhaa, kusafirisha nje na kuingiza pesa za kigeni." Amesema Waziri Jafo.
Akizungumzia sekta ya Viwanda katika miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia, Waziri Jafo ameeleza kuwa mwaka 2021 wakati Rais Samia anaingia madarakani, Idadi ya Viwanda ilikuwa 52, 128 na hadi kufikia mwaka 2025 kumeshuhudiwa Ongezeko kubwa la Viwanda, vikifikia 80, 000 huku Mkoa wa Pwani akiutaja kama Kinara kwa uwepo wa Viwanda vingi.
Kutokana na Ongezeko hilo la Viwanda, Waziri huyo ameeleza kuwa kwasasa Tanzania imeanza kuondokana na kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi, akieleza kuwa hamasa ya Rais Samia katika uwekezaji imesababisha Viwanda vilivyokuwepo kuongeza uzalishaji na hivyo nchi kuwa na utoshelevu wa bidhaa mbalimbali ikiwemo Bati, Nondo pamoja na saruji ambapo mahitaji yake ni Tani Milioni 8 kwa mwaka na uzalishaji wake sasa umefikia Tani Milioni 10 kwa mwaka.