Monday , 28th Jul , 2025

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewasili mjini St. George’s, nchini Grenada jana Jumapili, Julai 27, 2025 akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la nne wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum – ACTIF 2025).

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewasili mjini St. George’s, nchini Grenada jana Jumapili, Julai 27, 2025 akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la nne wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum – ACTIF 2025) linaloanza leo Julai 28–30, 2025 katika kituo cha mikutano cha Radisson.

Mkutano huo mkubwa unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Afrika na visiwa vya Karibiani na una kaulimbiu inayosema: “Uhimilivu na Mabadiliko: Kuimarisha Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Afrika na Karibiani katika Kipindi cha Changamoto za Kidunia.”

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki Mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali, kukutana na viongozi wa mataifa mengine, pamoja na kushiriki katika mikutano na wawekezaji wakubwa.

Baadhi ya maeneo muhimu ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo ni kuanzishwa kwa eneo la Biashara Huria kati ya Afrika na Karibiani, kuimarisha baraza la biashara la Afrika na Karibiani, kuchochea uchumi na ubunifu pamoja na Kukuza uhusiano wa usafiri wa anga na baharini kati ya Afrika na Karibiani.

Mkutano huo umeratibiwa na Jamhuri ya Granada pamoja na taasisi ya kifedha ya kimataifa yenye lengo la kukuza biashara ya bidhaa na huduma ndani na nje ya Afrika (Afreximbank).