Thursday , 3rd Jul , 2025

Msanii maarufu wa muziki wa Afrobeats kutoka Nigeria, Burna Boy  ametangaza kuachia albamu yake mpya iitwayo "No Sign Of Weakness" ambayo inatarajiwa kutoka rasmi tarehe 11 Julai 2025.

Albamu hiyo mpya itakuwa na jumla ya nyimbo 16, na mashabiki wake duniani kote wanaisubiri kwa hamu kubwa. Kilichowashangaza wengi ni tangazo la Burna Boy la kuandaa ziara ya kimataifa (world tour) ya albamu hiyo, hata kabla ya kutoka rasmi. Hili limechukuliwa kama uthibitisho wa imani kubwa aliyonayo katika kazi yake mpya na jinsi mashabiki walivyo na matarajio makubwa.

"No Sign Of Weakness" inatajwa kuwa ni mwendelezo wa ufanisi wa Burna Boy katika kulitangaza bara la Afrika kupitia muziki wake duniani. Albamu hii inatarajiwa kuangazia mchanganyiko wa mitindo ya kisasa ya muziki na miziki ya asili ya Kiafrika, sambamba na ujumbe wa uimara, ushindi, na utambulisho wa mtu.

Mashabiki wanashauriwa kufuatilia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii kwa taarifa zaidi kuhusu orodha ya nyimbo (tracklist), tarehe rasmi za ziara hiyo, na mahali albamu itakapopatikana mara baada ya kutoka.