
Wimbo huu mpya umeshika kasi kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya muziki, huku mashabiki wakifurahishwa na ujumbe, ubora wa utunzi, na mchanganyiko wa ladha ya muziki wa kizazi kipya na ule wa zamani.
“Ebenezer” ni kazi inayoonyesha ukomavu wa wasanii hawa wakongwe waliotengeneza historia ndefu katika muziki wa Afrika Mashariki. Ukisikiliza kwa makini, wimbo huu ni simulizi ya maisha, shukrani, mafanikio na changamoto, ukiwa umebebwa na sauti tamu ya Q Chief pamoja na mistari mikali ya Professor Jay na Chameleone.
Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya pili kwa Professor Jay na Chameleone kushirikiana kwenye wimbo — mara ya kwanza ikiwa ni kwenye kibao maarufu "Ndivyo Sivyo", kilichotoka zaidi ya miaka 11 iliyopita na kuacha alama kwenye muziki wa ukanda huu.
Wimbo wa Ebenezer unaibua hisia kali kwa wasikilizaji wakongwe na wapya, na kuonesha kuwa mastaa hawa bado wana nafasi kubwa katika ramani ya burudani Afrika Mashariki.