Sunday , 30th Mar , 2025

Imeelezwa kuwa asilima 80 ya vifo duniani husababishwa na magonjwa yasiyoambukizwa na ajali (NCDs). Ripoti hiyo imetolewa na Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Jamii, Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kongamano la Healthy Cities kwa mwaka 2025 lililofanyika jijini Paris,

Wakati wa kuhitimisha kongamano hilo la Healthy Cities kwa mwama 2025, miji mitatu kati ya miji wanachama 74 imetambuliwa kwa mafanikio na hatua kubwa walizopiga katika kuzuia magonjwa yasiyoambukiza na ajali.

Miji hiyo ni mji wa Córdoba nchini Argentina, mji wa Fortaleza wa nchini Brazil, na mji wa Greater Manchester wa nchini Uingereza ambapo imetunukiwa tuzo kwa mafanikio yao katika utekelezaji wa sera mbalimbali na hatua madhubuti za kulinda na kuboresha afya ya jamii, ikiwa kama miji ya mfano wa kuigwa kwa miji mingine duniani.

Dkt. Krug, alisisitiza umuhimu wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, hasa katika kipindi hiki ambapo Dunia inapitia changamoto na vikwazo vingi katika sekta ya afya. Alibainisha kuwa ipo haja ya mshikamano wa kimataifa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs). Aidha, aliendelea kueleza kuwa serikali za miji, hasa mameya na timu zao, zina nafasi nzuri ya kutekeleza sera madhubuti za afya kwa jamii zao.

“Kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na usalama wa barabarani ni changamoto, lakini tunapiga hatua na tunaona matokeo chanya,” alisema Dkt. Krug. Alisisitiza umuhimu wa kutumia data na ushahidi wa kisayansi ili kupima maendeleo na kuboresha sera kwa wakati.

Ushirikiano wa  miji inayofuata misingi na kanuni za Afya ya Jamii yaani Healthy Cities ni programu inayosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kusaidiwa na Bloomberg Philantorpies na Vital Stratergies. Programu hii inajumuisha miji ipatayo 74 duniani kote, inayopata msaada wa kitaalam kutekeleza afua za afya ya jamii. Ni miji 16 pekee kutoka Afrika iliyopo katika programu hii, ikiwa ni pamoja na jiji la Kigali Rwanda, Nairobi Kenya na jiji la Kampla Uganda. Jiji la Kigali limeonekana kupiga hatua kubwa katika kuboresha njia za watembea kwa miguu, ikiwa ni juhudi za kuboresha afya ya jamii na usalama maeneo ya mijini.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO asilimia 82 ya vifo vya mapema kutokana na magonjwa yasiyoambukiza hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Miji iliyopo kwenye programu ya Healthy Cities inaendelea kuboresha sera zao mbalimbali ili kuweka mazingira wezeshi ya mijini na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza.

Tanzania, licha ya kwamba haina jiji mwanachama katika programu ya Healthy Cities, tayari imeanza kuchukua hatua madhubuti ya kuboresha sera zake kama mpango kuweka mazingira wezeshi ya wananchi kufanya mazoezi na pia kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa. Kwa sasa katika jiji la Dar es Salaam kila Jumamosi kuanzia saa 12 mpaka saa 3 asubuhi ni siku ya kufanya mazoezi na kupunguza matumizi ya magari hivyo daraja maarufu la Tanzanite hufungwa ili kuruhusu wananchi kuweza kufanya mazoezi kwa usalama. Mpango huu unasimamiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa.