Akizungumza katika uzinduzi wa vivuko hivyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema vivuko vilivyozinduliwa siku ya Jumatano tarehe 22 Januari 2025, vitaungana na vingine viwili ambavyo vinafanya kazi tayari na kufanya jumla ya vivuko vinne. Pia, amesema kufikia Mei mwaka huu, Azam Marine wataongeza vivuko vingine vinne na kufanya jumla ya vivuko kuwa vinane.
Kwa mujibu wa Ulega, kila kimoja kati ya vivuko hivyo vina uwezo wa kubeba abiria 250 kwa wakati mmoja na kutumia dakika sita kwa safari moja. Kwa wastani huo, ndani ya saa moja, kivuko kimoja kinaweza kubeba mpaka abiria 2500. Kwa vivuko vinane, maana yake abiria zaidi ya 20,000 wanaweza kusafirishwa ndani ya saa moja.
“Historia imeandikwa. Huu ndiyo ushirikiano wenye manufaa baina ya serikali na sekta binafsi. Kipekee kabisa, naomba nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ubunifu wake na maelekezo yake kwetu kuhusu kushirikiana na sekta binafsi kuondoa kero za wananchi ndiyo zinaleta mambo kama haya,’ amesema.