Wednesday , 6th Nov , 2024

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miezi sita jela au kulipa shilingi 40,000 kwa kila mmoja jumla ya Watanzania 64 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 31302/2024 ya kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za uhamiaji.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 6, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Beda Nyaki baada ya washtakiwa kukiri kosa lao na mahakama kutiwa hatiani kwa kosa hilo.

Waliohukumiwa adhabu ni Abdallah Ramadhani, Abdul Rajab, Abdulrahman Mtimbe, Abdul Lusambi, Abubakary Kitemba, Ally Maduka, Adam Mkumba, Akida Ally, Ally Ally na wenzao 54.

Washtakiwa hao baada ya kuhukumiwa adhabu hiyo, walishangilia kwa kupiga makofi wakiwa ndani ya mahakama ya wazi namba moja, wakifurahia kupigwa faini ya shilingi elfu 40.

Hata hivyo washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na kukwepa adhabu ya kwenda kutumikia kifungo cha miezi sita jela.